STAND UNITED YA SHINYANGA WALIVYOKABIDHIWA BASI JIPYA NA KAMPUNI YA JAMBO
Mashabiki wa timu ya Stand United ‘Chama la Wana’ wamefunga mitaa mbalimbali mjini Shinyanga takribani saa nne wakifurahia kukabidhiwa basi la kisasa lenye thamani ya shilingi milioni 200 kusaidia timu hiyo lililotolewa na Kampuni ya vinywaji baridi ya Jambo Food Products inayomilikiwa na Salum Hamis maarufu ‘Jambo’.
Basi hilo aina ya Mercedes Benz lenye namba za usajili T841 DHY limekabidhiwa leo Jumanne Januari 9,2018,katika kiwanda cha Jambo Food Products na kushuhudiwa na mashabiki wa timu hiyo ambao mara baada ya zoezi la makabidhiano waliingia mtaani wakiandamana kwa magari,pikipiki na bajaji.
Akikabidhi basi hilo kwa uongozi wa timu ya Stand United,mkurugenzi wa kampuni hiyo,Salum Hamis alijigamba na kudai kuwa basi hilo ni la kisasa hakuna timu yoyote nchini inayomiliki basi kama hilo.
“Hili basi aina ya Mercedes Benz,hakuna timu yenye basi kama hili ambalo lina viti vinavyoweza kutumika kama kitanda,klabu zingine hadi zile kongwe zinatumia mabasi aina ya Youtong tu”,alisema Hamis.
“Leo nimetimiza ahadi niliyotoa ya kununua basi kwa ajili ya timu yetu,naamini litatumika kama motisha kwa wachezaji wetu ili kuhakikisha timu hii inafanya vizuri katika michezo,naahidi kuendelea kutoa misaada pale itakapohitajika kusaidia timu hii,pia naomba tushirikiane kutangaza kampuni ya Jambo Group”,aliongeza.
Nao viongozi wa timu hiyo,mwenyekiti wa Stand United,Dkt. Ellyson Maeja,nahodha wa timu Erick Muliro na Kocha mkuu wa timu hiyo Amas Nyangabo waliishukuru kampuni hiyo kwa kuwafadhili gari hilo ambalo watalitumia katika shughuli mbalimbali za kimichezo ikiwemo kusafirisha wachezaji.
Furaha ya usafiri kwa timu hiyo iliyokuwa imepotea kwa kipindi kirefu ikajionesha dhahiri pale mashabiki wake walipofanya maandamano wakipita kila mtaa kufurahia ufadhili wa basi hilo huku askari polisi wa usalama barabarani wakitanda katika kila barabara kuhakikisha maandamano hayo yanakuwa ya amani.
Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked

X